Machweo nyuma ya majengo.

WAANDISHI WA HABARI WA RADIO JAMII WAPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI WA MGUSO

Mwenyekiti wa vyombo vya habari vya kijamii Tanzania Ngugu John Baptist amefungua mafunzo leo katika hotel ya Royal village mjini Dodoma.

Na: Bakari Khalid

Waandishi wa habari wa radio jamii wametakiwa kutumia mafunzo wanayopatiwa ili kuleta matokeo chanya katika vituo vyao vya utangazaji.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari vya Kijamii (TADIO), John Baptist Mutesasira, wakati akifungua mafunzo ya uongozi wa mguso kwa vyombo vya habari vya kijamii.

Baptist amesema kuwa radio ni nyenzo kuu ya kufikisha taarifa kwa umma. Kwa mujibu wa ripoti ya watafiti wa usikilizaji wa vyombo vya habari – IPSOS, radio ina nafasi kubwa katika jamii, hivyo ni jukumu la waandishi wa habari kuhakikisha wanatumia maarifa haya kwa weledi ili kuboresha uendeshaji wa vituo vyao.

Muwezeshaji wa mafunzo ndugu Jopseph Paniel ,akitoa maelekezo kwa washiriki wa mafunzo leo katika hotel ya Royal village mjini Dodoma.

Awali, akimkaribisha mwenyekiti, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Joseph Paniel, alisisitiza kuwa radio jamii ina mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii. Aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kuongoza vyombo vya habari vya kijamii.

Mafunzo haya yanajumuisha mada mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa vituo vya radio, uongozi thabiti, mbinu za kuongeza ushirikishwaji wa jamii katika vipindi vya radio, na matumizi ya teknolojia mpya katika utangazaji wa habari. Washiriki pia wanapata nafasi ya kufanya mazoezi ya vitendo ili kuhakikisha wanapata uelewa wa kina kuhusu dhana ya uongozi wa mguso.

Washiriki wa mafunzo katika vikundi wakijadiliana na kubadilishana uzoezi wakati wa mafunzo katika hotel ya Royal Village mjini Dodoma leo.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu wanayoipata itawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ushawishi wa vyombo vya habari vya kijamii katika kuhamasisha maendeleo. Wamesisitiza kuwa radio jamii zina mchango mkubwa katika kuelimisha na kutoa sauti kwa jamii zisizo na fursa za kutosha katika vyombo vikubwa vya habari.

Mafunzo haya ya siku mbili, yanayofanyika katika Hoteli ya Royal Village  mkoani Dodoma, yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la UZIKWASA na Mtandao wa Vyombo vya Habari vya Kijamii Tanzania -TADIO ambayo  yanatarajiwa kukamilika kesho, tarehe 25 Machi 2025.