Machweo nyuma ya majengo.

JAMII FM YASAIDIA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI MITAMBO KUJENGEWA MADARASA.

Majengo ya madarasa kabla
Majengo ya madarasa baada

Wanafunzi wa shule ya msingi Mitambo kata ya Madimba halmashauri ya wilaya ya Mtwara, waliokuwa wakisomea chini ya mikorosho na kwenye mabanda yaliyoezekwa kwa makuti baada ya jamii fm kutoa taarifa zinazoihusu shule hiyo mnamo tarehe 19/01/2018, wameondokana na adha hiyo, baada ya serikali na wadau wengine wa elimu kuchangia ujenzi wa madarasa matano na Ofisi moja ya mwalimu.

Baada ya kusota kwa kipindi kirefu wakiwa chini ya miti na katika vibanda vya nyasi kuitafuta elimu wakichomwa na jua, Wanasema ukiona mateso yanazidi basi ujue neema hukaribia, hakika ndivyo ilivyokua kwa wanafunzi 229 wa shule ya msingi Mitambo waliokua wanalazimika kusomea chini ya miti na katika vibanda vya nyasi kwa kukosa madarasa.

Leo hii jambo hilo limegeuka historia, baada ya serikali kuelekeza jitihada zake katika shule hiyo na kuamua kukamilisha vyumba vitano vya madarasa ili kuwafanya wanafunzi wa shule hiyo kuwa na furaha

Kero ya kusomea nje haikuwa kwa wanafunzi peke yao, bali hata kwa walimu pamoja na wazazi wa wanafunzi hao.

Halmashauri ya wilaya ya Mtwara ina shule za msingi 67 zilizosajiliwa ambapo kati ya hizo, shule kumi zinakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Shule ya Mitambo ilianzishwa mwaka 2009, ambapo mwaka 2015 walihitimu wanafunzi wa darasa la saba kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa.

KILICHOTOKEA BAADA YA SHULE YA MITAMBO KURIPOTIWA

Mnamo tarehe 21/01/2019 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara QS Omary Kipanga, alizungumza na waandishi wa habari juu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Mitambo iliyopo kata ya Madimba ambayo iliripotiwa kuwa na madarasa ya makuti, unaendelea shuleni hapo.

Akizungumza na mwandishi wa habari Kipanga amesema ujenzi huo ni wa vyumba vitatu vya madarasa ambao serikali inasimamia, na kimoja ambacho kinajengwa kwa nguvu ya wananchi, pamoja na nyumba ya mwalimu.

“Vyumba vipo na vya matofali na vimeezekwa majengo matatu, lakini kuna ujenzi ambao unaendelea kwa nguvu za wananchi wa darasa moja, lakini na sisi halmashauri katika bajeti yetu ya mwaka 2017/18 tumetenga bajeti kwa ajili ya madarasa mawili na nyumba ya mwalimu, mpaka sasa vyumba vya madarasa vinavyotumika ni vyumba vitatu, vingine vitatu vipo kwenye ujenzi”, amesema Mkurugenzi Kipanga.

Sambamba na hilo Mkurugenzi amekiri uwepo wa upungufu wa walimu, ambapo amesema tatizo hilo ni la nchi nzima na sio kwenye halmashauri yake peke yake, hata hivyo serikali inafanya jitihada za kutatua changamoto hiyo.

“Tuna changamoto ya walimu sio kwenye halmashauri yangu tu, ni nchi nzima, kwa sababu mimi katika halmashuri yangu nina upungufu karibu mia 5 na kitu, pale walimu 7, wanafunzi 437 na madarasa 7 yaani la kwanza mpaka la saba”, ameendelea kufafanua Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wa elimu ya sekondari Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara amesema ana tatizo kubwa la kuwepo kwa upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, kwani kwenye halmashauri yake ina uhaba wa walimu 71 wa masomo ya sayansi.

“Kwa upande wa sekondari masomo ya sanaa hatuna tatizo sana, ila kwa masomo ya sayansi mimi kwenye halmashauri yangu ina upungufu wa walimu takriban 71 kwa shule zote, lakini bado tuna mikakati ya kuhakikisha tunapata walimu wa mazoezi ili tuweke priority kwenye masomo ya sayansi”, amesema Mkurugenzi huyo.

Tarehe 21/05/2019 Taarifa ya serikali mwaka mmoja baadae Serikali ilikuja na ufafanuzi kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kutokana na kuendelea kusambaa kwa taarifa zilizotolewa na jamii fm katika ukurasa wake wa facebook, taarifa hiyo inavyopatikana katika tovuti ya serikali http://moe.go.tz/sw/component/k2/item/2230-taarifa-kwa-umma-juu-ya-majengo-ya-shule-ya-msingi-mitambo.html  ikiwa na ujumbe kama ifuatavyo:

Kumekuwa na taarifa inayosambaa kwenye mtandao wa Instagram inayoonesha majengo ya Shule ya Msingi ya Mitambo iliyo Kata ya Madimba Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kutoa taarifa kwamba majengo hayo siyo yanayotumika katika Shule hiyo kwa sasa.

Shule hii ina usajili Namba EM14873 na ina madarasa ya kudumu ambayo yamejengwa na Serikali kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo na Halmashauri ya Wilaya husika. Kama ilivyo katika shule za maeneo mbalimbali nchini ujenzi wa madarasa pamoja na matundu ya vyoo zaidi bado unaendelea na kwa kumbukumbu za Wizara, majengo hayo ya tope yaliyooneshwa katika Mtandao kwa sasa hayapo katika shule hiyo.

Uwepo wa mafanikio haya, Jamii fm na wadau wake wanazidi kupata nguvu ya kuweza kupaza sauti za maeneo yaliyopo vijijini ili kuhakikisha huduma nzuri katika Nyanja mbalimbali inapatikana