Machweo nyuma ya majengo.

KUHUSU CHINA KUTOA MSAADA TANZANIA


Ubalozi wa China nchini Tanzania umeipatia Serikali msaada wa vifaa kinga kwa ajili ya kuendelea kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 (Corona), na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kukabiliana na ugonjwa huo, hadi hapo utakapomalizika.

Akipokea vifaa hivyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema msaada huo utaenda kwa watumishi wa afya kote nchini kwani serikali imetoa kipaumbele cha kwanza kwao ili kuweza kuwakinga na maambukizi ya Covid-19. “kwa niaba ya serikali tunaishukuru sana Serikali ya China kwa mchango huu, na niendelee kuwathibitishia wale wote mnaoisaidia Serikali ya Tanzania,msaada huu tutaupeleka kwa watumishi wa afya,kipaumbele ni kuwakinga watumishi wa afya wasipate maambukizi”

Ummy Mwalimu amesema msaada huo uliotolewa na ubalozi wa China nchini Tanzania ni pamoja na mavazi (PPE) 1,000 ya kujikinga wakati wa kuhudumia watu waliothibitika kuwa na ugonjwa wa corona, Barakoa (Mask) 100,000 pamoja na Vipima joto vya mkono(thermal scanner) 150.

Kwa upande wake balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Wang Ke amesema nchi yake na Tanzania ni marafiki kwa muda mrefu na ugonjwa huo ulipoikumba Nchi yao kwa mara ya kwanza, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono katika mapamabana dhidi ya ugonjwa huo, hivyo na wenyewe wamejitoa kuisaidia kukabiliana nao.

Mhe.Wang Ke amesema Serikali ya China kwa sasa imechukua hatua na kujitoa rasmi kuwa nchi itakayoisaidia Tanzania katika misaada ya dharura ya vifaa kinga ambayo itasaidia kuweza kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Katika mwendelezo wa kuisadia vifaa kinga Serikali ya Tanzania, kwa mara nyingine tena inatarajia kupokea msaada wa vifaa tiba vya kusaidia wagonjwa kupumua (Ventilator) 500 kutoka kwa mfanyabiashara raia wa China Jack Ma.

Credit #JamiiForum