HABARI MAELEZO KUSHIRIKIANA NA TADIO

MKURUGENZI wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbasi, amesema idara yake ipo tayari kushirikina na Asasi ya Habari za Maendeleo Tanzania (TADIO), katika kuhakikisha wananchi wanaoishi vijijini, wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Dk. Abbasi alisema hayo hivi karibuni alipotembelea ofisi za TADIO zilizopo katika majengo ya Makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine alilenga kufahamu kile ambacho Asasi hiyo inafanya.

“Tupo tayari kushirikiana nanyi katika kufikia malengo yenu ya kutangaza habari za maendeleo, hususan vijijini” alisema Dk. Abbasi.

Dk. Abbasi ambaye aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi, Patrick Kipangula, alisema idara yake ipo tayari kutoa elimu kuhusu sheria ya huduma za vyomba habari kwa wananchama wa TADIO kupitia majukwaa mbalimbali ili wawe na uelewa mpana.

Awali akimkaribisha Dk. Abbasi, Mwenyekiti wa TADIO Prosper Kiwigize aliomba ushirikiano kutoka serikalini, ili asasi hiyo kupitia wanachama wake ambao ni Redio zenye maudhui ya kijamii, iweze kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati.

Alisema, kumekuwepo na ushirikiano duni kutoka miongoni mwa maofisa habari katika halmashauri mbalimbali nchi, hali inayokinzana na jitihada za serikali ya awamu ya tano katika kufikia malengo ya Tanzania ya viwanda.

Kwigize pia alimuomba Dk. Abbasi kuangalia upya namna ambavyo Redio zenye maudhui ya kijamii, zinavyoweza kunufaika na matangazo kutoka serikalini, lakini pia aliomba kuboreshwa kwa taratibu za upatikanaji wa vitambulisho vya wanahabari (press cards), hususani kwa wanaandishi wa habari vijijini.

“Waandishi wa habari waliopo vijijini, wamekuwa wakiingia gharama kubwa kupata vitambulisho ‘press cards’, tunaomba hili ulitafutie ufumbuzi,” alisema Kwigize.

Akizungumzia kuhusu matangazo, Dk. Abbasi alisema, kumebuniwa utaratibu mpya ambapo MAELEZO itafanya pia kazi ya kuwa wakala wa matangazo ya serikali hivyo kuwepo kwa uratibu mzuri.

“Mfumo holela uliopo wa utoaji wa matangazo ya serikali, umeleta shida kubwa sana. Yapo matangazo ambayo hayalipiki kwa kuwa yalitolewa bila kuwepo kwa bajeti. Tunakuja na mfumo mpya,” alisema Dk. Abbasi.

Aidha, Dk. Abbasi alliitaka TADIO kuhamasisha waandishi walipo kwenye redio wanachama wake, kujiendeleza kielimu, ili kufikia kiwango cha stashahada (diploma), kitakachotambuliwa na serikali ifikapo mwaka 2021.

“Tunataka uandishi wa habari uwe taaluma rasmi, hivyo sheria inaelekeza ifikapo 2021, kiwango cha chini cha elimu kiwe Diploma. Wahamasisheni waandishi wenu waende shule,” alisema Dk. Abbasi.

Kwa upande wa vitambulisho vya waandishi wa habari, Mkurugenzi Msaidizi, Kipangula alisema utaratibu wa upatikanaji wake utaboreshwa zaidi baada ya kukamilika kuundwa kwa Bodi ya Ithibati. Chini ya Bodi hiyo, vitambulisho hivyo vitapatikana kwa urahisi zaidi kwakuwa vitatumia mfumo wa kielektroniki.

Kipangula pia alitoa wito kwa waandishi wa habari kusoma wenyewe sheria ya huduma ya vyombo vya habari (MSA), badala ya kusubiri kusomewa.

Ziara hiyo ni kwanza kwa Mkurugenzi wa MAELEZO kutembelea ofisi za TADIO tangu ilipoanzishwa Agosti 2017, imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili.