
Mtandao wa Vyombo vya Habari vya Jamii nchini Tanzania TADIO kwa ufadhili kutoka Vikes imepanga kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA kutoka redio jamii wanachama wa TADIO ambao watawajibika kuhakikisha kuwa vituo vyao vya redio vinarusha matangazo yake mubashara kupitia tovuti ya kurusha matangazo mubashara ya TADIO itakayozinduliwa hivi karibuni. Hii imesemwa na Afisa Mradi wa TADIO, Bi Saumu Bakari wakati wa mafunzo ya kwanza kati ya matano ya jinsi ya kutumia tovuti hiyo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Leo tumeanza na ninyi lakini tutafundisha vituo vyote vya redio chini ya mwavuli wa TADIO juu ya jinsi ya kutumia tovuti hii. Ombi langu kwenu ni kuitumia tovuti hii vyema kwani imetengenezwa mahsusi kwa ajili ya vituo vya redio vya wanachama wa TADIO ili waweze kuwafikia watazamaji zaidi,” akaongeza Bi Saumu.

Kwa upande wake, Bwana Peik Johansson kutoka Vikes alisisitiza kufuata kanuni za uandishi bora wa habari zitakazochapishwa kwenye tovuti hiyo. Alisema kuwa, kichwa kizuri cha habari na habari yenyewe ikiwa ya kuvutia na picha yenye maelezo mazuri yatafanya habari yako isomwe zaidi.
Naye Bwana Markku Liukkonen kutoka Vikes alifundisha juu ya urushaji wa matangazo ya redio mubashara kupitia tovuti hiyo na jinsi ya kufanya ili vituo vyao vya redio viweze kurusha matangazo hayo. Bwana Markku pia aliwafundisha juu ya jinsi ya kusasisha habari zao kwenye tovuti hiyo. Bwana Markku aliwaambia kwamba wanapaswa kuwafundisha waandishi wa habari wengine juu ya jinsi ya kutumia tovuti hiyo ili waweze kuchapisha habari zao wenyewe.
“Sasa tumewafundisha na mmekuwa wasimamizi wakuu wa kurasa zenu. Mna uwezo wa kuongeza watumiaji zaidi ambao watachapisha habari zao wenyewe hivyo kuwapunguzia mzigo. Ikiwa mnakabiliwa na changamoto yoyote, msisite kuwasiliana na mimi au Ayubu au Amua – tutakuwa tayari kuwasaidia,” alisema.

Bwana Christian Kilewa kutoka Redio Jamiii Kilosa ambaye alihudhuria mafunzo hayo, aliwashukuru TADIO na Vikes kwa mafunzo hayo na kuiomba TADIO kufanya semina kwa wamiliki wa redio juu ya umuhimu wa bandari hii ili wao (wataalamu wa TEHAMA) wapate msaada kamili kutoka kwao. “Nimefurahi sana kwa fursa hii kwani hatujawahi kurusha matangazo yetu mubashara katika kituo chetu. Tunaomba TADIO kuwaelimisha wamiliki wetu wa redio juu ya umuhimu wa kurusha matangazo mubashara ili waweze kutoa ufadhili na msaada kwa redio.” Alisema.
Baada ya mafunzo haya, wakufunzi wa eneo hilo Ayubu Lulesu na Bwana Amua Rushita watatembelea vituo vya redio ambavyo vilihudhuria mafunzo hayo ili kutatua changamoto mbalimbali walizokumbana nazo. Mafunzo haya ni moja kai ya matano yatakayofanywa na VIkes yenye lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA wa redio washirika wa TADIO juu ya kuchapisha habari na kurusha matangazo mubashara kupitia tovuti hiyo.