Machweo nyuma ya majengo.

RAIS WA ZANZIBAR APONGEZA RADIO JAMII

RADIO Jamii iliyopo Micheweni Pemba imepongezwa kwa mchango wake mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii juu ya tahadhari ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona kisiwani humo.

Pongezi hizo zimetolewa wakati viongozi wa Mikoa miwili ya Pemba walipokutana na na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein huko Ikulu ndogo, Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Akisoma taarifa ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkuu wa Mkoa huo Omar Khamis Othman alisema kuwa Redio Jamii iliyopo Micheweni imeweza kutoa vipindi mbali mbali ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa, umuhimu wa kunawa maji tiririka na sabuni kama njia ya kujihadhari na ugonjwa huo.

Kiongozi huyo alieleza kuwa jumla ya wananchi 7,689 wananoishi maeneo ya kisiwa cha Fundo, Kokoa, Njau, Kojani, Makangale,Kifundi, Msuka, Micheweni, Shanake na Kiuyu kwa Manda, Tondooni, Tumbe, Shumba Mjini, Maziwa Ngombe, Michenzani, Kiuyu Mbuyuni wamepata elimu ya kuelewa ugonjwa wa Corona na hatua za kujikinga na ugonjwa huo.

Alieleza kuwa redio hiyo imeweza kusaidia jitihada hizo za kutoa elimu katika maeneo hayo yakiwemo yale ya visiwa na maeneo mengineyo ikiwa ni pamoja na kueleza katika vipindi vyake juu ya umuhimu wa kutoa taarifa pale wanapogundua kuna mtu ama watu wameingia kutoka nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa huo alieleza kuwa elimu iliyolenga kuutambua ugonjwa wa Corona na mbinu zote muhimu za kujikinga na ugonjwa huo imetolewa kupitia mikutano ya jamii kwa Shehia 61 za Mkoa wa Kaskazini Pemba.

More >> Micheweni FM