Rais wa Zanzibar aipongeza UNESCO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi ameipongeza azma ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulkia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa jengo la Beit al Ajaib baada ya kuporomoka sehemu kubwa ya jengo hilo hivi karibuni.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tirso Dos Santos.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza Mwakilishi huyo wa (UNESCO) kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Shirika hilo, hivyo hatua yake hiyo ya kuinga mkono Zanzibar katika kulifanyia matengenezo jengo la Beit al Ajaib ni uthibitisho mkubwa.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kuchukua hatua za makusudi mara tu baada ya kutokea tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuunda Kamati ya Uchunguzi ya sababu zilizopelekea kuanguka kwa jengo hilo la Beit al Ajaib huku yeye mwenyewe akikutana na Wadau wa Mji Mkongwe kujadili tukio hilo kwa azma ya kutafuta ufumbuzi.

Rais Dk. Mwinyi alitoa ushauri kwa Shirika la (UNESCO) wa kuyafanyia tathmini majengo yote ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ili yasiendelee kuleta athari zaidi.

Chanzo: Ukurasa wa Facebook wa Ikulu Zanzibar