
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na
kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Pamoja na hotuba hii ninawasilisha vitabu
vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2020/21. Taarifa hizi ndiyo msingi wa bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2020/21 nitakayowasilisha hapa Bungeni leo jioni.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya njema.
Aidha, naendelea kumshukuru kwa kulijalia Taifa letu amani, utulivu na
mshikamano na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa 19 na wa mwisho wa
Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya
kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba
nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea kuliongoza vema Taifa
letu. Kwa kipindi hiki cha miaka minne na nusu ya utawala wake tumeshuhudia
kuimarika kwa uchumi, mfumuko wa bei umedhibitiwa, miradi mikubwa ya maendeleo
inatekelezwa, uwajibikaji katika utumishi wa umma umeimarika na kero za wananchi
wanyonge zinatatuliwa. Kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini
kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango tangu mwanzo wa uongozi wake hadi sasa.
4.
Mheshimiwa Spika, vile
vile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb),
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao kwa uongozi wao mahiri
wameendelea kumshauri vema Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa.
5.
Mheshimiwa Spika,
Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa
kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na
Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Mollel (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais
kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie nafasi hii kutoa salamu za pole
kwako, Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa ujumla kwa kuondokewa na
Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini
(CCM), Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude
Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa Richard
Mganga Ndassa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), na Mheshimiwa Balozi
Dkt. Augustine Philip Mahiga, Mbunge wa kuteuliwa (CCM) aliyekuwa Waziri wa
Katiba na Sheria. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
Amina!
7.
Mheshimiwa Spika, nchiyetu imepata mvua nyingi zilizo juu ya
wastani hali iliyopelekea kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali.
Mafuriko haya yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazao ya wakulima, mali na
miundombinu hususan barabara, reli na madaraja. Mafuriko hayo yameathiri
utelekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza gharama za ukarabati wa
miundombinu iliyoharibika. Kwa msingi huo, katika mwaka 2020/21 kipaumbele ni
kukarabati miundombinu iliyoharibika.
8.
Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, nchi yetu na dunia kwa ujumla ilikabiliwa
na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaojulikana kama COVID – 19
inayosababishwa na virusi vya Corona. Ni dhahiri kuwa ugonjwa huu umeathiri
uchumi wa nchi nyingi duniani kutokana na vifo, kuongezeka kwa gharama za
utoaji huduma katika sekta ya afya na kuathiri shughuli za biashara na
uzalishaji hususan kwa nchi zinazotegemea utalii.
9.
Mheshimiwa Spika, jambo jema ni kuwa nchi yetu haikuathirika sana na
ugonjwa huu kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama Taifa tuliendelea kumtegemea Mwenyezi
Mungu, kuchukua tahadhari za kiafya kama inavyoshauriwa na wataalam pamoja na
kufanya kazi kwa bidii. Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kukabiliana na ugonjwa huu ambapo hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha shilingi
bilioni 15.49 kwa ajili ya ununuzi wa
vifaa tiba na kinga. Hatua nyingine ni pamoja na: kutolewa msamaha wa kodi kwa
aina 15 za vifaa vya kupambana na COVID – 19; kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga
na maambukizi; kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uangalizi kwa wasafiri
wanaoingia nchini na wanaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huu; na kuanzishwa
kwa huduma ya namba maalum ya kupiga simu bila malipo kwa ajili ya msaada wa
kiafya. Vile vile, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua
mbalimbali za Sera ya Fedha ili kulinda na kuimarisha uchumi zikijumuisha:
kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa
kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 7 hadi 6; kushusha kiwango cha
riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu kutoka asilimia 7 hadi 5;
kupunguza kiwango cha dhamana za Serikali kutoka asilimia 10 hadi 5 kwa dhamana
za muda mfupi na kutoka asilimia 40 hadi 20 kwa hati fungani; na kuzielekeza
kampuni zinazotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha
miamala kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 3 hadi 5 na kiwango cha
akiba kwa siku kwa wateja kutoka shilingi milioni 5 hadi 10.
10. Mheshimiwa
Spika, kutokana na hatua
madhubuti zilizochukuliwa na Serikali, hivi sasa hali imeimarika ambapo
shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kufanyika kama awali. Serikali
imeruhusu vyuo vikuu vimefunguliwa, wanafunzi wa kidato cha sita wamerudi
shuleni kujiandaa na mitihani, shughuli za michezo yote zimeruhusiwa, anga limefunguliwa ambapo ndege za mizigo na
abiria zinaendelea kuingia nchini na hivyo kupokelewa kwa watalii kutoka nchi
mbalimbali. Hii ni ishara dhahiri ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais kwa Taifa
hususan katika kipindi cha majanga na misukosuko mikubwa kwa dunia kama ugonjwa
huu.
11. Mheshimiwa Spika, Taarifa
ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Mwaka 2020/21 zimezingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa wadau katika hatua
za uandaaji na maamuzi katika ngazi zote Serikalini. Nitambue mchango mkubwa wa
Bunge lako Tukufu chini ya uongozi wako Mheshimiwa Job
Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa
Mashimba Mashauri Ndaki (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti
na wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa ushauri makini waliotupatia. Ushauri wao umezingatiwa
kikamilifu katika uandaaji wa taarifa nilizowasilisha mbele ya Bunge hili.
12. Mheshimiwa Spika, maandalizi
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 yamezingatia vipaumbele vya
Serikali ya Awamu ya Tano vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015
na ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alizotoa wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja.
Aidha, katika mwaka 2020/21 msukumo mkubwa utawekwa katika kukamilisha
utekelezaji wa miradi inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa.
MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2019
Uchumi wa Dunia
13. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2020, uchumi
wa duniaulikua kwa asilimia 2.9
mwaka 2019. Aidha, uchumi wa dunia unakadiriwa kuporomoka na
kufikia ukuaji wa asilimia hasi 3.0 mwaka 2020 ambao kwa kiasi kikubwa utachangiwa
na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID – 19. Katika mwaka 2021 uchumi wa
dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.8 kutokana na
matarajio ya kutoweka kwa virusi vya Corona katika nusu ya pili ya mwaka 2020
na hatimaye, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi duniani ikijumuisha biashara na
uzalishaji viwandani na utekelezaji wa sera za kuongeza ukwasi katika nchi
mbalimbali.
Uchumi
wa Afrika na Kikanda
14.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa nchi za AfrikaKusini mwa Jangwa la Sahara, kasi ya
ukuaji wa uchumi ilifikia asilimia 3.1 mwaka 2019. Matarajio ya ukuaji wa
uchumi ni kupungua na kufikia wastani wa asilimia hasi 1.6
mwaka 2020 kutokana na athari za mlipuko wa
ugonjwa wa COVID – 19. Aidha, ukuaji wa uchumi katika nchi za ukanda huo,
unatarajiwa
kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2021. Ongezeko hilo
litatokana na jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID – 19, matarajio ya
kuongezeka kwa misaada kutoka nchi zilizoendelea kwa ajili ya kupambana na
ugonjwa huo na matarajio ya utulivu wa bei ya nishati ya mafuta katika soko la
Dunia.
15.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2019, uchumi wa nchi za ukanda wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki uliendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa na ukuaji wa
asilimia 7.0, Rwanda asilimia 9.4, Uganda (asilimia 4.9) na Kenya asilimia 5.4.
Aidha, kutokana na athari za COVID-19, ukuaji wa uchumi wa ukanda wa nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kupungua kidogo kwa mwaka 2020 na
hatimaye kuanza kuimarika mwaka 2021 kutokana na juhudi zinazochukuliwa na nchi
wanachama katika kupambana na athari za COVID-19 zikiwemo hatua za kifedha na
kibajeti pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za
uchukuzi (reli, barabara na madaraja) maji, nishati, elimu na afya.
Uchumi
wa Taifa
Pato la Taifa
16.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2019, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 kama
ilivyokuwa mwaka 2018. Ukuaji huu ulitokana na uwekezaji hususan katika
miundombinu ikiwemo: ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege; kutengamaa
kwa upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji;
kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na
kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Sekta zilizokua kwa viwango
vikubwa katika kipindi hicho ni pamoja na uchimbaji madini na mawe (asilimia
17.7), ujenzi (asilimia 14.8), sanaa na burudani (asilimia 11.2), na usafirishaji
na uhifadhi mizigo (asilimia 8.7). Kwa mwaka 2020, ukuaji wa Pato la
Taifa unatarajiwa kupungua kidogo kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 hadi
5.5 kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania hususan kuhimiza wananchi waendelee kufanya kazi wakati
wanachukua tahadhari dhidi ya corona kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya
pamoja na matarajio ya kuimarika kwa uchumi wa kikanda na dunia.
17.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2019, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi
2,577,967 ikilinganishwa na shilingi 2,452,406 mwaka 2018, sawa na ongezeko la
asilimia 5.1. Vile vile, Pato la wastani kwa kila mtu katika dola za Marekani
liliongezeka hadi kufikia dola za Marekani 1,121 mwaka 2019 kutoka dola za
Marekani 1,078 mwaka 2018.
Mwenendo
wa Bei
18.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2019, mwenendo wa
mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika wigo wa
tarakimu moja ambapo ulifikia wastani wa asilimia 3.4 ikilinganishwa na wastani
wa asilimia 3.5 mwaka 2018. Mfumuko wa bei za nishati
umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 Aprili 2020 kutoka asilimia 13.3
Aprili 2019 kutokana na kupungua kwa bei za nishati ya mafuta katika soko la dunia.
Utekelezaji
wa Sera ya Fedha 2019/20
19. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia
Benki Kuu imeendelea kutekeleza sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi
ambayo imesaidia kupunguza viwango vya riba katika masoko ya fedha hususan riba
za mikopo na amana.
Wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha Julai 2019
hadi Aprili 2020 ulipungua hadi asilimia 16.85 ikilinganishwa na wastani wa
asilimia 17.16 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19, na riba za mikopo ya
kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.24 kutoka
asilimia 17.79. Vile vile, wastani wa riba za amana kwa ujumla ulikuwa asilimia
7.02 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, ikilinganishwa na wastani
wa asilimia 7.62 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19. Aidha, riba za amana
za kipindi cha mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77
katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 kutoka wastani wa asilimia 8.21
katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.
Ujazi
wa Fedha na Karadha
20. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2019 hadi
Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3)
uliongezeka kwa asilimia 9.9 na kufikia shilingi trilioni 28.8 mwezi Aprili
2020 kutoka shilingi trilioni 25.6 mwezi Aprili 2019. Ongezeko hili la ujazi wa
fedha ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, ongezeko la mikopo
kwa sekta binafsi pamoja na rasilimali fedha za kigeni katika sekta ya benki.
Mwenendo
wa Mikopo kwa Sekta Binafsi
21. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta
binafsi ulikuwa asilimia 8.7 kufikia shilingi trilioni 19.7 ikilinganishwa na
shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli
binafsi (asilimia 31.1) ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 17.6, uzalishaji
viwandani asilimia 11.0 na kilimo asilimia 7.7.
Sekta ya Nje
22. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, urari wa jumla wa
malipo ulikuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 897.1 ikilinganishwa na
nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019.
Hii ilichangiwa na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma
na uhamisho wa mali nchi za nje kulikotokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa
nje ya nchi.
23. Mheshimiwa Spika, nakisi kwenye urari wa biashara ya
bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje ulipungua hadi kufikia dola za
Marekani milioni 333.3 mwezi Aprili 2020, ikilinganishwa na nakisi ya dola za
Marekani bilioni 1.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua huku
kulitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hususa katika bidhaa
asilia na zisizo asilia kama vile dhahabu.
24. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, mauzo ya bidhaa na
huduma nje yaliongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 8.6 ikilinganishwa na
dola za Marekani bilioni 7.3 Aprili 2019. Hii ilichangiwa na kuanzishwa kwa
masoko ya madini nchini kulikopelekea kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu sanjari
na ongezeko la bei katika soko la dunia. Thamani ya uagizaji bidhaa na huduma
kutoka nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani bilioni 8.6, ikilinganishwa na dola
za Marekani bilioni 8.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Sehemu kubwa
ilitumika katika uagizaji mafuta na bidhaa za mitaji ikiwemo mitambo na mashine
inayotumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli,
barabara, madaraja na uzalishaji umeme.
Akiba ya Fedha za Kigeni
25. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, akiba ya fedha za
kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3, kiasi kinachotosheleza kulipia
uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1.
Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la miezi 4.0, ambayo ni juu ya lengo la
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua 6.0.
Mwenendo wa Thamani ya Shilingi
26. Mheshimiwa
Spika, thamani ya shilingi ya
Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani imeendelea kuwa tulivu kwa
kipindi chote cha mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili
2020, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa kati ya shilingi
2,299.3 na shilingi 2,302.7 katika soko la fedha la jumla ikilinganishwa na
wastani wa kati ya shilingi 2,276.4 na shilingi 2,300.9 kwa dola moja ya
Marekani katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.
Deni la Serikali
27. Mheshimiwa Spika, hadi
Aprili 2020, deni
la Serikali lilifikia shilingi trilioni 55.43. Kati ya kiasi hicho, deni la nje
lilikuwa shilingi trilioni 40.57 na deni la ndani shilingi trilioni 14.85. Deni
la Serikali lilichangiwa na kupokelewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia
miradi mbalimbali ya maendeleo inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi. Matokeo ya
tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2019, imeonesha kuwa deni la
Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Utafiti
wa Sekta Isiyo Rasmi
28. Mheshimiwa
Spika, mwaka 2019/20, Serikali
ilifanya utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kubaini
mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa kwa kutumia makadirio ya mapato na
ongezeko la thamani ya uzalishaji wa bidhaa na huduma kutoka shughuli za kilimo
na zisizo za kilimo; tija katika uwekezaji; kiwango cha ukuzaji mtaji; kutambua
mahali biashara zilipo; thamani ya uzalishaji kwa kila mtu; ajira na mgawanyo
wake; na mahusiano kati ya Sekta Isiyo Rasmi na sekta nyingine za kiuchumi.
29. Mheshimiwa
Spika, matokeo ya utafiti huo
yanaonesha kuwa: Mkoa wa Dar es Salaam una wamiliki wa shughuli za Sekta Isiyo
Rasmi wapatao 1,023,520 ambapo asilimia 47.6 wanajihusisha na biashara ya jumla
na rejareja pamoja na matengenezo ya magari na pikipiki; uwekezaji wa mitaji katika sekta isiyo rasmi
ni shilingi bilioni 901.5 kwa mwaka 2019; jumla ya ongezeko la thamani kwa mwaka katika bidhaa na
huduma zinazozalishwa katika sekta isiyo rasmi ni shilingi trilioni 6.2; na ajira katika sekta
isiyo rasmi kwa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi imepungua kutoka watu
1,208,250 (asilimia 61.5) mwaka 2014 hadi 1,154,336 (asilimia 55.2) mwaka 2019.
Hii inatokana na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupanua wigo
wa kujenga uchumi wa viwanda ambao matokeo yake ni kukuza upatikanaji wa kazi
zenye staha (decent work) na
kuongezeka kwa ajira katika sekta rasmi.
30. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya kina kuhusu
hali ya uchumi yapo katika Aya ya 9 hadi 26 ya hotuba yangu na kitabu cha Hali
ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019.
MAFANIKIO
YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2019/20
31. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha
miaka minne na nusu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17 – 2019/20),
yamepatikana mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo
yakiwemo:
(i)
Ukuaji wa Uchumi: uchumi wa Taifa uliendelea kuimarika ambapo ulikua kwa
wastani wa asilimia 6.9 na mfumuko wa bei kuendelea kupungua na kubaki katika wigo
wa tarakimu moja, chini ya wastani wa asilimia 5.0;
(ii)
Reli:Ujenzi wa reli ya
kati ya standard gauge unaendelea
ambapo, ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia
76.63 na kwa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 28. Hadi
Mei 2020, ujenzi wa reli ya standard
gauge umetumia shilingi bilioni 170, pamoja na dola za Marekani bilioni
1.5. Mradi huu umezalisha takribani ajira 13,117 na zabuni zenye thamani ya
shilingi bilioni 664.7 kwa kampuni za ndani;
(iii)
Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Kazi zilizokamilika ni pamoja naujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi
(njia ya kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji,
mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba
2; utafiti wa miamba na udongo; na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit tunnel) wenye urefu wa mita 147.6
na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja ambapo utekelezaji wa mradi wote
umefikia asilimia 10.74. Aidha, jumla ya shilingi trilioni 1.42 zimetumika
kugharamia mradi na ajira zipatazo 3,897 zimezalishwa;
(iv)
Nishati:
kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka
Makambako – Songea ambapo shilingi bilioni 160.1 zimetumika; kuendelea na
ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga
ambapo utekelezaji umefikia asilimia 67 na shilingi bilioni 219.4 zimetumika;
kuendelea na utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA
ambapo shilingi trilioni 2.27 zimetumika jumla ya vijiji 9,112 kati ya vijiji
12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa umeme, sawa na asilimia 74.3. Hadi Mei
2020, kiwango cha upatikanaji wa umeme (overall
electricity access rate) kimefikia asilimia 84.6 kutoka asilimia 67.8 mwaka
2016;
(v)
Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Serikali imeendelea kuboresha Shirika la Ndege kwa
kununua ndege mpya 11. Kati ya hizo, ndege nane (8) zenye thamani ya shilingi
trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa
ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3) yamefanyika ambapo ndege mbili
(2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash 8-400;
(vi)
Viwanja vya Ndege: kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Ndege vya
Mwanza awamu ya kwanza, Nachingwea na Kilimanjaro (KIA); kuendelea na ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya Geita (asilimia 78) na Songea (asilimia 34). Aidha,
ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere umekamilika na kuanza kutumika ambapo kiasi cha Euro milioni 276
sawa na takribani shilingi bilioni 722.1 zilitumika;
(vii)
Bandari: kukamilika
kwa ujenzi wa Gati Na.1, 2, 3, 4 na Gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro)
katika bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika
bandari ya Mtwara umefikia asilimia 61; na kukamilika kwa uongezaji wa kina cha
bandari ya Tanga na ujenzi wa Gati namba 2 umefikia asilimia 60. Aidha, kwa upande wa Bandari za Maziwa Makuu: katika
Ziwa Victoria – ujenzi wa magati
ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine
na Gati la majahazi Mwigobero umekamilika; kununuliwa kwa vifaa vya kuhudumia
mizigo na meli; na ukarabati wa majengo na ofisi za bandari. Ziwa Tanganyika
– uboreshaji wa Gati la Kagunga umekamilika; ujenzi wa Gati la Sibwesa
umefikia asilimia 98; ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Kabwe
umefikia asilimia 56; na ujenzi wa
miundombinu na Gati la Bandari ya Lagosa umefikia asilimia 53. Ziwa Nyasa – ujenzi wa sakafu ngumu kwa
ajili ya maegesho katika bandari ya Kiwira; na ujenzi wa Gati la Ndumbi
umekamilika;
(viii) Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa
Makuu: kukamilika kwa ujenzi
wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika
Ziwa Nyasa, ukarabati wa meli ya MV Victoria katika ziwa Victoria na meli ya
mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika; kukamilika kwa asilimia 98 ya
ujenzi wa Chelezo na MV Butiama asilimia 98; na kuendelea na ujenzi wa meli
mpya (MV Mwanza) yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo
katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji umefikia asilimia 60;
(ix)
Barabara na Madaraja: ujenzi wa Barabara:
kukamilika kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa jumla ya
kilometa 2,624.27 na kuendelea na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami
zenye urefu wa kilometa 1,298.44; barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi
Kibaha (km 19.2) umefikia asilimia 80; na ujenzi wa Ubungo Interchange umefikia asilimia 77. Madaraja: kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya Mfugale (Dar es
Salaam), Magufuli katika mto Kilombero (Morogoro), Momba (Rukwa), Sibiti
(Singida), Mara (Mara), Lukuledi (Lindi), Mangara (Manyara) na Kavuu (Katavi);
kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kitengule (Kagera) asilimia 50, Ruhuhu
(Ruvuma) asilimia 86, Msingi (Singida) asilimia 40, New Wami (Pwani) lenye urefu wa mita 513.5 na barabara unganishi
zenye kilomita 4.3 umefikia asilimia 39 na daraja jipya la Selander lenye urefu
wa kilomita 1.03 na barabara unganishi zenye kilomita 5.2 umefikia asilimia
38.2; na kuanza kwa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu
wa kilomita 3.2 ambapo malipo ya awali
ya shilingi bilioni 61.4 yamefanyika.
(x)
Kilimo, Mifugo na Uvuvi: katika Kilimo,
miche bora ya korosho 12,252,197 imezalishwa na mbolea tani 519,813 imesambazwa
katika mikoa 26 ya Tanzania Bara; na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora
za mahindi, ngano, maharage, mpunga, soya, alizeti, mtama, ufuta, viazi
mviringo na mazao ya bustani kufikia tani 49,040.66. Aidha, kupitia Mradi wa
Kuongeza Uzalishaji wa Mpunga (ERPP), shughuli zifuatazo zimetekelezwa: ukarabati
wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Kigugu – Mvomero (hekta 200) asilimia 50, Mvumi – Kilosa
(hekta 249) asilimia 84, Kilangali – Kilosa (hekta 600) asilimia 51, Msolwa
Ujamaa – Kilombero (hekta 675) asilimia 40 na Njage – Kilombero (hekta 325) asilimia
84. Mifugo: kuendelezwa kwa mashamba
matano (5) ya kuzalisha mitamba; kuzalishwa na kusambazwa kwa mitamba 15,097 ya
ng’ombe wa maziwa; kununuliwa na kusambazwa kwa lita 8,823.53 za dawa aina ya Paranex ya kuogesha mifugo; kukarabatiwa
kwa majosho 1,129; na kutolewa kwa chanjo ya ndigana kali (east coast fever) kwa ng’ombe 70,260. Uvuvi: uzalishaji wa vifaranga 15,041,401 vya samaki; na kuongezeka
kwa uvunaji wa samaki (maji ya asili) kufikia tani 470,309.23;
(xi)
Miradi ya Afya: ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini
ikijumuisha vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za rufaa za
mikoa 10 na zahanati 1,198; kuongezeka kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 269
mwaka 2019/20; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za
Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), Burigi –
Geita, Mwananyamala – Dar es Salaam na hospitali za rufaa za kanda ya kusini
Mtwara, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi
wa Kituo Maalum cha kutenga wagonjwa wa magonjwa yanayoambukiza (Isolation Centre) katika hospitali ya
Taifa Muhimbili, Temeke, na Maabara ya Taifa Mabibo; na ununuzi wa dawa,
chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ikijumuisha vifaa tiba vya kisasa
katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
(xii)
Miradi ya Elimu: kukamilika na kuanza kutumika kwa Maktaba ya Kimataifa
yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam; kuendelea na ujenzi wa maabara ya masomo ya Sayansi katika Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Kampasi ya Solomon Mahlangu), ujenzi wa hosteli
za Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hosteli za
wanafunzi na Maktaba katika Chuo Kikuu Mzumbe (kampasi ya Mbeya); utoaji wa
mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 365 mwaka 2015/16
hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20; uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza
ujuzi kwa vijana nchini; na ukamilishaji wa maboma 364 ya nyumba za walimu wa
shule za msingi kwenye maeneo yenye mazingira magumu na kuendelea kugharamia
elimumsingi bila ada ambapo shilingi trilioni 1.03 zimetumika kuanzia mwaka
2015 hadi Mei 2020.
(xiii)
Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: Serikali imeendelea kuboresha huduma za maji safi na
salama vijijini na mijini ambapo miradi 1,423 (vijijini 1,268 na mijini 155)
imetekelezwa na kukamilika kati ya mwaka 2015 na 2019. Miradi hiyo inajumuisha:
mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa,
Tabora, Igunga, Uyui na Nzega ambapo ujenzi wa matanki 17 na ulazaji wa mabomba
makubwa ya kusafirisha maji kutoka kijiji cha Solwa – Nzega – Tabora – Igunga
(km 290.7) umekamilika. Utekelezaji wa miradi ya maji umewezesha kiwango cha
upatikanaji wa maji kufikia asilimia 70.1 vijijini na asilimia 84 mijini;
(xiv) Madini: Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na marekebisho ya
sheria na mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini na hivyo kuanzishwa kwa
Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati
ya Serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); na
kufanyika kwa malipo ya fidia ya dola za Marekani milioni 100 kutoka Kampuni ya
Barrick ikiwa ni sehemu ya kwanza ya kiasi cha makubaliano ya awali ya
kulipa fidia ya dola za Marekani milioni 300. Aidha, marekebisho ya Sheria
yamewezesha kuanza kwa majadiliano baina ya Serikali na Makampuni yote makubwa
ya madini kwa lengo la kupata asilimia 16 ya hisa kwa Serikali. Mafanikio
mengine ni kuanzishwa kwa masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini nchini;
kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bukoba,
Handeni, Bariadi na Musoma; kukamilika kwa ujenzi wa viwanda viwili (2) vya
mfano vya kuchenjua dhahabu vya Lwamgasa na Katente; kukamilika kwa ujenzi wa one stop center Mirerani, kuimarika kwa
udhibiti wa madini ikijumuisha ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliowezesha kupungua kwa utoroshaji madini; na kuongezeka kwa maduhuli ya Serikali kutoka
shilingi bilioni 196 mwaka 2015/16 hadi zaidi ya shilingi bilioni 470 mwaka
2019/20; na
(xv)
Uendelezaji wa Viwanda: kufanikisha ujenzi wa viwanda vipya 8,477 ambapo viwanda
vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Mafanikio
mengine ni pamoja na upanuzi wa Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi cha
Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani).
32. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya kina kuhusu
mafanikio ya utekelezaji wa Mpango yapo katika Aya ya 32 na 33 ya hotuba yangu
na Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Kipindi cha Mwaka 2016/17
hadi 2019/20.
MPANGO
WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21
Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa Mwaka 2020/2133. Mheshimiwa
Spika, Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2020/21 umezingatia shabaha kuu za uchumi jumla zifuatazo:
(a)
Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa unatarajiwa kupungua
kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2020
ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019. Hii
ni kutokana na athari za ugonjwa wa COVID-19 ulioenea katika nchi nyingi ambazo
ni washirika wetu wakubwa wa kibiashara;
(b)
Kuendelea
kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki katika wigo wa
tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3 hadi 5 kwa mwaka 2020/21;
(c)
Mapato ya ndani kufikia
asilimia 14.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0
mwaka 2019/20;
(d)
Matumizi ya
Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21;
(e)
Nakisi ya bajeti
(ikijumuisha misaada) kuwa asilimia 2.6 mwaka 2020/21 ikiwa ni chini ya
asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki; na
(f)
Kuwa na akiba ya
fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na
huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.0.
Miradi ya Kipaumbele 2020/21
34. Mheshimiwa
Spika, mwaka huu nchi yetu
imepata mvua nyingi zilizosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu. Katika
mwaka 2020/21, Serikali itaweka kipaumbele katika ukarabati wa miundombinu ya
kiuchumi na kijamii iliyoharibiwa na mvua ikijumuisha barababara na madaraja,
reli, nguzo za umeme, mabwawa ya maji na majengo ya taasisi za afya na elimu;
35. Mheshimiwa
Spika, miradi na shughuli za
kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo:
(a)
Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi
wa Viwanda: Katika eneo hili mkazo
utawekwa kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi
nchini. Miradi mahsusi katika eneo hili ni pamoja na:
(i)
Uendelezaji wa Viwanda ikijumuisha kuendeleza vituo vya utafiti wa teknolojia na bidhaa za
viwandani vya CAMARTEC, TIRDO, TEMDO na SIDO; kuboresha Shirika la Nyumbu; na uendelezaji
wa maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bunda, Manyoni, Tanga, Mtwara, Dodoma, Bagamoyo
na Benjamin William Mkapa;
(ii)
Kilimo: kuboresha
utafiti na miundombinu ya utafiti katika kilimo; kuongeza tija katika
uzalishaji kwa kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo, huduma za
ugani, maghala na masoko kwa mazao ya kimkakati ya michikichi, kahawa, pamba,
chai, tumbaku na miwa; kujenga na kukarabati miundombinu ya skimu za
umwagiliaji; na kuboresha huduma za ushauri kuhusu utafiti, mafunzo na
usambazaji wa taarifa za kilimo;
(iii)
Mifugo: kuimarisha tiba na udhibiti wa magonjwa ya mifugo;ujenzi wa majosho; kuboresha miundombinu ya
uhifadhi wa chanjo; kuimarisha vituo vya uhimilishaji Kitaifa na Kikanda; na
kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo;
(iv)
Uvuvi: kujenga
na kukarabati miundombinu ya ufugaji wa viumbe maji; kuboresha Shirika la Uvuvi
Tanzania (TAFICO); kujenga na kukarabati miundombinu ya mialo na masoko ya
uvuvi; na ujenzi wa bandari ya uvuvi; na
(v)
Madini: kujenga
ofisi nane (8) za maafisa madini na kituo cha umahiri; kujenga ghala la
kuhifadhi sampuli za miamba choronge (core
shed); kununua vitendea kazi kwa ajili ya shughuli za utafiti wa ikolojia; na
kununua vifaa vya maabara na utafiti;
(b)
Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa katika mwaka 2020/21
itajielekeza katika maeneo yafuatayo:
(i)
Elimu: kuendelea
kusomesha kwa wingi wataalamu kwenye fani na ujuzi adimu kama vile udaktari,
mafuta na gesi, Jiolojia, Jemolojia na Uhandisi migodi; kuendelea kugharamia
utoaji wa elimumsingi bila ada; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya
kujifunzia na kufundishia katika shule na vyuo vya ualimu na vya Elimu ya Juu; ujenzi
wa nyumba 122 za walimu katika shule 10 za msingi na shule 20 za sekondari katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi; na kuendelea
kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu;
(ii)
Afya: kuendelea na ujenzi wa hospitali 71 za wilaya;kuboresha miundombinu ya kutolea huduma
za afya katika Hospitali za Rufaa za mikoa, kanda na Taifa; kuimarisha
usambazaji wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya
kutolea huduma za afya; kuimarisha huduma katika Taasisi ya Saratani Ocean
Road, Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(MOI); kujenga na kukarabati vyuo vya Maendeleo ya Jamii; kuboresha uhai na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto; na kuboresha huduma za Ustawi wa Jamii;
(iii)
Maji: kuendelea
na ukamilishaji na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya Mikoa na
Wilaya ikijumuisha Mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Njombe, Katavi na Songwe;
kuendelea na ujenzi wa miradi ya maji ya Masasi – Nachingwea, Same – Mwanga –
Korogwe, ziwa Victoria – Igunga, Nzega na Tabora, ziwa Victoria – Kahama –
Shinyanga; na kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini.
(c)
Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara
na Uwekezaji: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili italenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa
miundombinu wezeshi ili kurahisisha uendeshaji biashara na uwekezaji nchini.
Miradi hiyo ni pamoja na: kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati ya standard gauge; mradi wa kuzalisha Umeme
wa Julius Nyerere Rufiji – MW 2,115; na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania.
Miradi mingine inajumuisha:
(i)
Barabara na Madaraja: kuendelea na ujenzi wa barabara ya Tabora –
Ipole – Koga – Mpanda (km 370); Barabara ya Mbeya – Makongolosi – Rungwa –
Itigi – Mkiwa (km 577.9);
Kigoma – Kidahwe – Uvinza – Kaliua – Tabora (km 389.7); Kabingo – Kasulu –
Manyovu (km 260); Mtwara – Mingoyo – Masasi – Songea – Mbamba Bay (km 1,470.9);
Bagamoyo – Makurunge – Saadani – Tanga (km 246); Sumbawanga
– Mpanda – Nyakanazi (km 517.4); Usagara – Geita – Buzirayombo – Kyamyorwa (km 388); ujenzi wa barabara za mzunguko Dodoma (km 112.3); na
upanuzi wa Barabara ya njia nane (8) Kimara – Kibaha (km 25.7);
kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kigongo – Busisi (Mwanza), daraja jipya la
Selander, Mangara (Manyara), New Wami (Pwani) na Kitengule (Kagera);
(ii)
Reli: kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha
kimataifa cha standard gauge, kuendelea na ukarabati wa vichwa vya treni, mabehewa ya mizigo na
abiria pamoja na njia za reli ya kati na TAZARA;
(iii)
Nishati: kuendelea na ujenzi wa bwawa la kuzalisha Umeme katika mradi
wa umeme wa Julius Nyerere Rufiji – MW 2,115,
kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 –
North – West Phase I, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400
kutoka Singida – Arusha – Namanga, Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV
400 Rufiji – Chalinze – Kinyerezi, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo
wa kV 400 kutoka Chalinze – Dodoma, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV
220 Rusumo – Nyakanazi na kuendelea na
usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA; na
(iv)
Bandari: kuendelea nauboreshaji wa miundombinu ya bandari za Dar es Salaam, Tanga
na Mtwara pamoja na bandari za maziwa makuu; na
(v)
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Viwanja vya Ndege: kuendeleakuboresha
Shirika la Ndege Tanzania, uendelezaji wa viwanja vya ndege ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa Kiwanja kipya cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato – Dodoma.
(d)
Kuimarisha Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango: Miradi itakayotekelezwa inalenga kuimarisha mifumo na
taasisi za utekelezaji na usimamizi wa Mpango, kuongeza upatikanaji wa
rasilimali fedha za kutekeleza mpango na kuweka vigezo vya upimaji wa matokeo ya utekelezaji. Miradi hii
itajumuisha maeneo ya Utawala Bora hususan utoaji haki na huduma za kisheria, kuimarisha
miundombinu ya Mahakama na Bunge na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama.
36. Mheshimiwa
Spika, Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2020/21 utaendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha Muungano
wetu. Miradi itakayotekelezwa kwa pamoja Tanzania bara na Zanzibar ni pamoja na:
(i)
Mradi
wa Kikanda wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa
Bahari ya Hindi (SWIOFish) kwa lengo
la kuimarisha uvuvi wa bahari kuu;
(ii)
programu
ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kulinda mazingira ya fukwe katika
ukanda wa bahari kuu;
(iii)
Mpango
wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF III) ambapo shughuli zilizopangwa ni kuendelea kuongeza maeneo ya
utekelezaji kutoka 161 ya sasa hadi maeneo 187 katika Halmashauri zote Tanzania
Bara na Wilaya zote Zanzibar ambapo shughuli za miradi 2,505 ya kutoa ajira za
muda na kuendeleza miundombinu zitatekelezwa Tanzania Bara na miradi 204
zitatekelezwa Zanzibar; na
(iv)
Mradi
wa Kupitia Mifumo ya Ikolojia kwa lengo la kuongeza uvumilivu wa kuhimili mabadiliko
ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia katika
Wilaya za Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa
(Dodoma) na Kaskazini A, (Kaskazini Unguja).
Shehia zitakazonufaika na mradi kutoka Kaskazini A ni pamoja na Shehia
ya Matemwe Kijini, Matemwe Jugakuu na Matemwe Mbuyutende.
37. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya kina kuhusu
vipaumbele vya Mpango kwa Mwaka 2020/21 yapo katika Aya ya 35 na 36 ya hotuba yangu
na Sura ya Nne ya Kitabu cha Mpango.
Ugharamiaji wa Mpango 2020/21
38.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imetenga shilingi
trilioni 12.90, kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2020/21, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2020/21.
Kati ya kiasi hicho, shilingi
trilioni 10.16 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.74 ni fedha za nje. Kiwango kilichotengwa kinaendana na lengo la Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano la kutenga kati ya asilimia 30
na 40 ya bajeti yote kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
39. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya kina kuhusu
ugharamiaji wa Mpango kwa Mwaka 2020/21 yapo katika Aya ya 40 na 41 ya hotuba
yangu na Sura ya Tano ya Kitabu cha Mpango.
Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa za Utekelezaji
40. Mheshimiwa Spika, moja ya nyenzo muhimu ya kufikia malengo ya mipango ni
kuwa na mfumo madhubuti wa kufuatilia utekelezaji na matumizi ya fedha
zilizopangwa. Kwa kutambua hilo, Serikali imejipanga kufanya ufuatiliaji wa karibu
wa matumizi sahihi ya fedha za miradi na kukagua maendeleo ya shughuli zote za
utekelezaji wa miradi kwa lengo la kujiridhisha iwapo utekelezaji unaendana na
matarajio na kuhakikisha matokeo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa manufaa ya
Taifa. Katika kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali itaandaa
Mwongozo wa Kisera wa kusimamia shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
41. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango,
Serikali inazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za
Serikali kuimarisha mifumo ya ndani ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya
maendeleo; kutafsiri malengo na viashiria vya utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 katika Mipango na Bajeti za
kisekta kwa mwaka 2020/21; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya
maendeleo kila robo mwaka; kuwajengea uwezo watumishi katika tasnia ya
ufuatiliaji na tathmini; na kuandaa taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na programu, na kuziwasilisha Wizara
ya Fedha na Mipango. Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini
ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha na Mipango.
MAJUMUISHO
42. Mheshimiwa
Spika, utekelezaji wa Mpango huu utakuwa ni wa mwisho katika
utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wenye dhima
ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya
watu. Mafanikio yanayotarajiwa kutokana na utekelezaji wa Mpango ni pamoja na: kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na utengamavu wa
viashiria vya uchumi jumla; kuimarisha utoaji wa huduma za jamii zikijumuisha
maji, elimu, afya na umeme vijijini; kuimarika kwa mazingira ya biashara na
uwekezaji; na kuongezeka kwa ajira na kipato cha wananchi na hatimaye kupungua
kwa kiwango cha umaskini nchini.
HITIMISHO
43. Mheshimiwa
Spika, kwa niaba ya Serikali napenda
kuwashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Sekta Binafsi,
Washirika wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla kwa michango yao katika utekelezaji
wa Mpango na kujenga uchumi. Michango hiyo imewezesha kupatikana kwa mafanikio mkubwa
katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
44. Mheshimiwa
Spika, naomba nitoe shukrani
zangu za dhati kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote,
Wakuu wa Idara Zinazojitegemea na Wakala, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa
ushirikiano wao katika kutayarisha
taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2020/21. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango kwa kunisaidia kuboresha hotuba hii. Aidha, ninawashukuru
watendaji wote wa Wizara ya Fedha na
Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Doto M. James kwa kusimamia kikamilifu
maandalizi ya hotuba hii.
45. Mheshimiwa
Spika, kipekee niwashukuru
Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii na vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa
Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21
vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni www.mof.go.tz.
46. Mheshimiwa
Spika, baada ya maelezo hayo
naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa
Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21.
47. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.