Machweo nyuma ya majengo.

UNESCO na SDC wawajengea uwezo shirika la Habari za maendeleo – TADIO

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Uswiss SDC, linaendelea na kujenga uwezo kwa viongozi wa Shirika la Habari za Maendeleo Tanzania (TADIO) ambalo ni mwamvuli wa mtandao wa Radio za Kijamii Tanzania.

Bi. Rose Ngunangwa afisa mradi kutoka UNESCO akizungumza na washiriki kuhusu malengo ya mradi

Mafunzo hayo yanayofanyika Mjini Morogoro kwa muda wa siku tano yanalenga kuwezesha Radio za kijamii kujisimamia na kutoa huduma stahiki kwa jamii hasa vijijini ambako mfumo wa upashanaji wa habari unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo hali duni ya kiuchumi na mawasiliano.

Viongozi wa shirika hilo, wanajengewa uwezo wa kufahamu masuala kiutawala, utafutaji na usimamizi wa fedha, kutambua wadau na namna ya kushirikiana na jamii katika utekelezaji wa shughuli zake.

Ndugu Prosper Kwigize Mwenyekiti wa TADIO

Prosper Kwigize ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Radio za Kijamii Tanzania amesema TADIO imepiga hatua kubwa sana ukilinganisha na tulipotoka lakini bado kuna jitihada kubwa inahitajika ili kuweza kuvisaidia redio hizi za kijamii kuweza kujiendesha ipasavyo kwa kubuni miradi mbalimbali.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, kulia ni Cosmas Lupoja (mratibu wa shirika la TADIO) na Shaaban Makame (mweka hazina wa TADIO)

Wakati wa mafunzo hayo, TADIO imefanya zoezi la kutambua wadau muhimu ambao wakitumika vema suala la upashanaji habari na ukuzaji wa shirika hilo litafanikiwa.